Home Makala EXCLUSIVE: KUTANA NA MUSSA KISSALA KIJANA WA KITANZANIA ANAYETIKISA MPIRA WA KIKAPU...

EXCLUSIVE: KUTANA NA MUSSA KISSALA KIJANA WA KITANZANIA ANAYETIKISA MPIRA WA KIKAPU NCHINI ENGLAND

1224
0
SHARE

image-2d6ca14c9786d81fa9a5e7bd62f4252e9c519469286f3ba95cb00b3b4475de4d-VNa Baraka Mpenja, Dar es Salaam

+255 712461976

UNAPOZUNGUMZIA michezo maarufu duniani ukiacha soka lenye mashabiki kila kona ya sayari hii ya tatu, mpira wa kikapu ni moja ya michezo yenye wapenzi wengi duniani na unaendelea kukua siku hadi siku.
Nchini Tanzania soka limetawala kila kona, udhamini umeelekezwa zaidi katika mchezo huo na kuiacha michezo mingine kama mpira wa kikapu bila muelekeo.
Wapenzi wengi wa soka Tanzania wanaamini soka ndio kila kitu, japokuwa kwa muda mrefu timu za soka kuanzia ngazi ya klabu na timu za taifa, mpira uko upande wa kushoto.
Kuna mipango mibovu, wachumia matumbo, kukosa mfumo wa soka la vijana na udhaifu mwingi ambao kila kukicha tunauzungumzia.
Wakati vijana wenye vipaji vya soka wakihangaika kutafuta njia ya kutokea katika mfumo mbovu wa Tanzania, wapo watanzania wanaokula maisha nchi za watu.
Kikapu kimemnufaisha sana Mtanzania Hasheem Thabeet anayecheza ligi ya kikapu nchini Marekani, NBA.
Kwa muda mrefu, Thabeet aliyepanda hewani amekuwa akicheza Marekani na kusahau shida na ubabaishaji wa Tanzania. Amevuna hela za kutosha na kila anapokuja likizo nchini anaonekana mfalme.
Thabeet ni mtu aliyejitambua mapema na kuendeleza kipaji chake. Kwake aliona mpira wa kikapu ndio mpango mzima. Hakuwaza soka hata kidogo.
Tatizo la watanzania wengi wanakumbatia zaidi mchezo wa soka, wanasahau kuwa kuna mataifa maarufu duniani ambayo hayawekezi zaidi katika soka. Kuna watu maisha yao yanategemea mchezo wa riadha kama Wakenya na Waethiopia kwa Afrika, wengine hutegemea masumbwi, wengine netiboli, wengine muziki na michezo mingine mingi. Sio lazima soka tu.
Unaweza kuwa maarufu kwa mchezo mwingine tofauti na soka. Hakuna ulazima wa kung`ang`ania soka wakati limetupiga chini. Unaifahamu njaa iliyopo timu za kikapu, netboli, ngumi nchini Tanzania?.
Mtandao huu uliwahi kuzungumza na mchezaji wa Chelsea, mzaliwa wa Tanzania, Adam Nditi.
Moja ya kilio cha nditi ni uraia wa nchi mbii. Alisema kama serikali ya Tanzania itaruhusu uraia wa nchi mbili, yuko tayari kuichezea Taifa stars hata kesho.
Kuna kitu cha msingi alichozunguza Nditi. Alisema wapo watanzania wengi wanaoishi nchi za Ulaya na wana vipaji katika fani mbalimbali, lakini wanashindwa kulisaidia taifa kutokana na kukosekana kwa sheria inayoruhusu uraia wa nchi mbili.
Nditi alisema watanzania hawa wenye vipaji vikubwa hawawezi kurudi nyumbani kirahisi kwasababu ya maslahi mazuri wanayopata huko. Nani wa kurudi Bongo kwenye ubabaishaji wakati kuna maisha mazuri ulaya?.
Mtandao huu unaendelea kukuvumbulia vipaji vya Kitanzania vilivyofichika barani Ulaya.
Kuna kijana mmoja anaitwa Mussa Kissala. Ukisoma jina lake unakubali kirahisi kuwa ni jina la Kitanzania. Na kweli ana asili ya Kitanzania kwa asilimia 100
Musa ni kijana mwenye kipaji kikubwa kwenye mpira wa kikapu. Anaishi na wazazi wake nchini England. Lakini ni Mtanzania halisi kwasababu wazazi wake ni watanzania , tena mama ni mtu wa Songea na baba mtu wa Kigoma.

image-7d08913d401dda5bd080b9826976999231d20d44e8970582fb5777f5e6d68941-VMussa (kulia) akiwa na baba yake bwana Kissala

ILIKUWAJE AKAENDA ENGLAND?

Wazazi wa Mussa waliondoka Tanzania mwaka 1998 kwenda nchini Botswana kikazi, (hawakutaka kutaja kazi yao). Novemba 3, 1999 walimzaa kijana waliyempata jina la Mussa Kissala. Miaka mitatu baadaye (2002) waliondoka Botswana kueleka nchini England kikazi.
Mussa na wazazi wake wanakaa eneo moja la Crawley, West Sussex, nchini England. Hili ni eneo lililosheheni vipaji vikubwa vya mpira wa kikapu na ndio maana Mussa amepata nafasi ya kujifunza zaidi mchezo huu.
Mussa mwenye miaka 14 sasa ametumia muda wake mwingi kujifunza mpira wa kikapu na sasa ameanza kuona mwanga mbele yake na anaelekea kufuata nyayo za kaka yake, Hasheem Thabeet anayecheza ligi ya NBA nchini Marekani.

MUSSA ANACHEZA TIMU GANI?
Kwa sasa Mussa ni mwanafunzi wa sekondari. Anaichezea timu yake ya shule iitwayo “The Holy Trinity Church of England Secondary School”.
Timu hii juzi ilishinda mashindano ya `School Championship` chini ya miaka 14. Mbali na kucheza timu ya shule, pia kijana huyu anaichezea timu ya Worting Thunder na wiki iliyopita timu hii ilishika nafasi ya pili kwenye mashindano ya England ya mpira wa kikapu kwa vijana wa umri chini ya miaka 14. Pia anacheza timu ya mtaani ambayo inacheza fainali zake jumamosi mjini Brighton katika viwanja vya Brighton university.

Baada ya kuonesha kiwango cha juu katika mashindano hayo, Mussa anayeipenda Tanzania, amechaguliwa kuingia katika timu ya kombaini ya Sussex na sasa safari yake ni kuelekea kuichezea timu ya taifa ya England chini ya umri wa miaka 14.
Ukiangalia mafanikio haya ya Mussa katika kipindi hiki kifupi, unaona kabisa anaelekea sehemu nzuri. Hiki ni kipaji cha Kitanzania ambacho kinaweza kurudi nyumbani kama uraia wa nchi mbili utaruhusiwa.

image-4b705dc386d20bc59209666607f1da9b7378b1b79ffa67a382146479759543f3-VMussa Kissala akifanya vitu vyake uwanjani

NINI KIMEMFIKISHA MUSA KATIKA MAFANIKIO HAYO?

Katika mahojiano maalum,binamu yake, Fadhila Lemba anasema kuwa Musa ni mtu wa kuthubutu. Ni kijana mwenye mtazamo wa kufanikisha ndoto zake kwa juhudi kubwa.
Fadhila anasema: “ Musa akipenda kitu huwa anapenda kujifunza kwa muda wote na lazima aelewe tu. Hata kikapu amejifunza kwa muda mrefu na anaendelea kujifunza mpaka atakapomfikia kaka yake Hasheem au zaidi ya hapo.

KWANINI ALICHAGUA MPIRA WA KIKAPU NA SIO SOKA?

Musa anasema nchini England soka ni mchezo wenye wapenzi wengi na kila mtu anaangalia hapo. Ni ngumu sana kupata nafasi ya kucheza katika timu za soka nchini England, na ndio maana yeye akaamua kuchagua mpira wa kikapu ambao huumudu vizuri na kuwakimbiza wengi.
Hata hivyo, Musa anaamini kupitia mpira wa kikapu ataweza kutimiza ndito zake kuliko kuhangaika na mpira wa miguu wenye changamoto kubwa.

VIPI KUHUSU NDOTO ZAKE?

Musa anamtazama Hasheem Thabeet kama mtu mwenye mafanikio makubwa zaidi nchini Marekani. Kwa maana hiyo anataka kumfikia au kumzidi. Ni mtu mwenye ndoto kubwa katika mpira wa kikapu, ndio maana anafanya juhudi kubwa kuhakikisha anafika mbali.
Mbali na malengo ya kufika mbali katika mpira wa kikapu, kijana huyu ana ndoto za kuwa daktari.
JE, ANAPENDA MICHEZO MINGINE NJE YA MPIRA WA KIKAPU?
Baba yake Mussa anasema mwanae ni mchezaji na mpenzi wa mpira wa miguu. Tena ni shabiki mkubwa wa klabu ya Liverpool.
Hata binamu yake Mussa, Bi. Fadhila anakiri hili kwa kusema: “Hata juzi juzi Liverpool walipofungwa na Chelsea 2-0, niliongea na Mussa akanieleza kuwa licha ya kufungwa, ubingwa lazima uendee Liverpool”.
Pia anacheza michezo mingine kama vile kukimbia mbio za mita 200 na kurusha tufe. Kutokana na uwezo wake katika michezo, Musa alishawahi kupewa tuzo ya mwanamichezo bora wa shule yake.

image-ef3d956a23cbefdd01ca9e1b429708a6a3ee80183106f76dfcce243e474b8c05-VMussa Kissala ( wa pili kushoto) akiwa kwenye moja ya kikosi cha timu yake

JE, AMEWAHI KUJA TANZANIA?

Binamu yake Fadhila anasema kuwa Mussa anapenda sana Tanzania na mara nyingi wakati wa likizo anakuja kutembea.
“Hivi ninavyokwambia, Agosti 8 mwaka huu Mussa atakuja nchini Tanzania”. Anafafanua Fadhila Lemba.
Fadhila anacheka kidogo! Hahahah!, “Mussa na mimi tulizaliwa siku moja ya novemba 3, tofauti ni miaka tu. Tunapendana sana na mimi ndiye rafiki yake mkubwa, akija huwa anapenda kutoka na mimi kwenda kutembea”.

VIPI TABIA YAKE AKIJA TANZANIA?

Mussa ni kijana alijengeka katika misingi ya nidhamu kubwa. Fadhila anasema huwa anapenda sana kusoma, lakini muda mwingi anatamani kwenda kutemba hasa katika fukwe za bahari ili kupunga upepo wa Tanzania.
Fadhila anasema Musa anapenda sana kuogelea. Lakini kitu kimoja kinachomtofuatisha yeye na mdogo wake Swedi Kissala ni ukimya.
  Swedi ambaye ni mdogo wake Mussa anapenda sana kuongea ongea, lakini kwa Mussa ni tofauti.
“Anaongea, lakini sio kama mdogo wake . Ni mtu mtulivu sana”. Fadhila anamchambua binamu yake.

image-f3f231b71f7462b7b4f69841563ba483e56fb5820676d51ca503cd4fe2632c86-V (1)VIPI KUICHEZEA TIMU YA TAIFA YA TANZANIA YA MPIRA WA KIKAPU?

Hapa kuna tatizo. Fadhila anasema kila mara anamuuliza Mussa swali hili, lakini anaishia kusema labda!. Kijana huyu anasema yuko tayari kuja kucheza Tanzania kama wataruhusu uraia wa nchi mbili. Yaleyale ya Adam Nditi.

WAZAZI WAKE WANASEMAJE KUHUSU TANZANIA?

Musa na wazazi wake wanapenda sana Tanzania, hivyo baba yake Bwana Kissala anasema hakuna haja ya watanzania kutojua kuwa ni watanzania.
“Niliongea na baba yake akasema wanajivunia kuwa watanzania. Wanaipenda sana Tanzania. Hakuna haja ya kuficha”. Haya ni maneno ya Fadhila kwenye mahojiano maalum na mtandao huu.
Musa naye anaipenda sana Tanzania, anapenda kuja Tanzania, anapenda kukaa Tanzania.

UPI UJUMBE WA MUSA KWA TANZANIA?

Mussa anasema uraia wa nchi mbili ukiruhusiwa atarudi kucheza Tanzania kama kweli kuna mpira wa kikapu. Musa anapenda weledi katika kazi zake, hivyo kama Tanzania kuna mpira wa kikapu atarudi. Kijana huyu anaishauri serikali kufikiria jambo hili.

Huyu ndiye Musa Kissala, kijana mwenye kipaji kikubwa zaidi katika mpira wa kikapu. Siku si nyingi anatarajiwa kuonekana katika kikosi cha timu ya taifa ya England ya mpira wa kikapu ya vijana umri wa miaka 14 .
Kwa moyo wote, mtandao huu unamtakia kila la heri Musa katika maisha yake ya mpira wa kikapu.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here